Blogger Widgets
Home » » SEKONDARI ZA KATA HANDENI ZACHOCHEA MIMBA!!

SEKONDARI ZA KATA HANDENI ZACHOCHEA MIMBA!!


WANANCHI wilayani Handeni wameilalamikia mazingira magumu
kimiundombinu ya shule za sekondari za
kata katika wilaya hilo na kudai ndiyo
chanzo cha kuongezeka kwa mimba kwa
wanafunzi na kukatisha masomo. Kauli hiyo imetolewa kwa nyakati
tofauti katika mahojiano ya baadhi ya
wakazi wa Handeni na mwandishi wa
habari hizi ndani ya uchunguzi
uliofanywa hivi karibuni maeneo anuai
ya wilaya hiyo kwa ushirikiano na Chama cha Wanahabari Wanawake
(TAMWA). Abdulah Mwamponda Mkazi wa Kijiji cha
Msasa, wilayani Handeni alisema shule
nyingi za kata zimejengwa mbali na
makazi ya wanafunzi jambo ambalo
linawapa mzigo wazazi na wanafunzi
kujitafutia usafiri wa kwenda na kurudi shuleni. Alisema katika kijiji
hicho wapo
wanafunzi ambao hutembea umbali wa
kilometa 12 na hata 20 kila siku kuanzia
Jumatatu hadi Ijumaa kwenda na kurudi
shuleni, umbali ambao umekuwa na
vishawishi vingi hasa kwa wanafunzi wa kike kiusafiri. Alisema usafiri
katika vijiji hivyo ni wa
baiskeli na pikipiki (bodaboda) ambao
wazazi wengi wanashindwa
kugharamia hivyo watoto kutembea
kwa umbali huo, huku wakati mwingine
wakishawishika kupewa msaada wa lifti na madereva wa bodaboda ambao
baadaye huanza kushirikiana nao
kimapenzi. Mzazi Fatuma Shaban kutoka Kijiji cha
Komnyang'anyo alisema wanafunzi
wengi huondoka nyumbani kwao saa 10
za asubuhi na kurudi usiku kutokana na
umbali huo huku wengine wakishinda
shuleni bila chochote kutokana na uduni wa maisha ya kaya nyingi eneo
hilo. Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari
Kilimani, Rajab Nyange alisema katika
shule hiyo iliyopo Kata ya Vibaoni nje
kidogo ya Mji wa Handeni wapo
wanafunzi wanaotoka vijiji vya mbali
takribani kilimeta sita hadi 10 kutoka nyumbani kwao, ambao hutembea
kilomita 20 kila siku yaani kwenda na
kurudi shuleni jambo ambalo linaibua
vishawishi kwa wanafunzi. "Mzazi anashindwa hata kumpa mtoto
wake sh. 100 au 200 kila siku ya shule
kwa ajili ya kula chochote awapo
shuleni, je ataweza kumlipia mtoto huyo
gharama za usafiri ambazo ni za juu
zaidi kutokana na umbali kutoka kijiji kimoja hadi kingine," alihoji
Nyange. Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya
ya Handeni Hassan Mwachibuzi anasema
Ofisi yake haina taarifa za ubakaji wa
moja kwa moja japokuwa anakiri
kuwepo kwa vitendo vya utoro kwa
wanafunzi wote kwa sababu mbalimbali. Anasema pamoja na hayo
utoro waweza kuingiliana na
ukatishwaji masomo kwa mimba. Kiongozi huyu anakiri suala la umbali wa
shule huchangia vishawishi kadhaa vya
wanafunzi hasa wa kike kukumbwa na
vikwazo kadhaa katika masomo yao.
Hata hivyo anabainisha kuwa uongozi
unajitahidi kulitatua suala hilo kwa kuongeza ujenzi wa hosteli kwa
wanafunzi katika shule za kata ili
wanafunzi waondokane na vikwavyo
anuai. Aliongeza kuwa tayari wamejenga
hosteli katika maeneo ya Kisasa,
Kwamsisi, Misima, na kudai kuwa
wanaendelea maeneo mengine kwa
kushirikiana na wananchi na wahisani
huku lengo ni kuhakikisha kila kata inakuwa na hosteli zake kwa ajili ya
wanafunzi wanaotoka maeneo ya mbali
na shule. Short URL: http://www.thehabari.com/? p=16959

0 comments:

Post a Comment

.